breaking news New
TFF na sheria zenye utata

TFF na sheria zenye utata

ADHABU YA ZAHERA.

Na Emmanuel M. Makalla

Kawaida kila familia, Taasisi, Kampuni au jamii yoyote ile lazima inakuwa na miiko, taratibu, tamaduni na kanuni zake katika kuendesha shughuli na maisha yao ya kila siku.

Kuhusu kanuni ya TFF/Bodi ya ligi inayoongelea mavazi ya benchi la ufundi katika michezo ya Ligi Kuu, Ligi Daraja la kwanza na Ligi Daraja la pili ni kanuni mpya ambayo imeongezwa na kuanza kutumika katika msimu mpya wa 2019/2020.

Kanuni yenyewe namba 14 (2m) (UTARATIBU WA MCHEZO) inasema hivi; nanukuu “Kocha Mkuu na viongozi wa Benchi la Ufundi wanawajibika kuvaa sare maalumu za timu yao kwa Benchi la Ufundi. Endapo Kocha Mkuu atahitaji kuvaa mavazi tofauti anawajibika kuwa katika mavazi ya Heshima na Nadhifu.”

Tuanze na kanuni yenyewe; Kwanza, kabisa kanuni hii ina mapungufu kwa maana kwamba kanuni kama hii inapotungwa inapaswa iwe na vifungu vidogo vinavyofafanua kanuni Kuu lakini hii ya kwetu iko kimya tu.

Mfano; katika hiyo kanuni ilitakiwa kuwe na kifungu kidogo kinachoelezea aina ya mavazi ambayo ni nadhifu na yenye heshima, ingeweza kutaja kwamba mavazi nadhifu kwa mjibu wa kanuni hii ni vazi la kitenge, gunia, kanzu, bukta, gauni, n.k. lakini kwa hii inaacha mwanya kwa wahusika. Kama mhusika anaona akivaa kaptura kama hiyo ya Zahera anapendeza basi anaweza kuvaa.

Pili, Bodi ya Ligi inapotunga kanuni kabla ya kuanza kuzitumia huwa inashirikisha wadau wake ambao ni vilabu vya Ligi Kuu, Ligi Daraja la kwanza na Ligi Daraja la pili na iwapo vilabu vitaona kwamba hizo kanuni ziko sawa basi ndipo Bodi ya ligi inazipeleka kwenye kamati ya utendaji ya TFF ambayo inazihakiki na kuzipitisha ili zianze kutumika.

Sasa iwapo vilabu vilishirikishwa katika kuandaa na kupitisha hiyo kanuni walitakiwa kuhoji aina gani ya mavazi kwa mjibu wa hiyo kanuni ni nadhifu na yenye heshima. Lakini kama waliacha iwe kimya basi TFF na Bodi ya Ligi wako kwenye nafasi ya kuamua ni aina gani ya mavazi ni nadhifu na yenye heshima pengine kulingana na mazingira na tamaduni za kitanzania. So adhabu ya Zahera iko sawa upande mmoja.

Sasa kutokana na mapungufu ya kanuni yenyewe na kwa vile tayari Zahera amehukumiwa kwa kutumia hiyo kanuni basi moja kwa moja hukumu yake itaendelea kutumika kama reference/rejea kwenye makosa mengine kama hayo.Kuhusu mijadala inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii.

Baada ya nyundo ya Bodi ya Ligi kutua kwa Mwinyi Zahera wadau mbalimbali wa michezo wamekuwa na maoni tofauti wengine wakitumia picha mbalimbali kuelezea hilo jambo hasa kwa kukosoa maamuzi ya Bodi ya Ligi.

Kuna picha inayoonyesha wachezaji wa Yanga pamoja na kiongozi wa Benchi la Ufundi la Ruvu Shooting aliyevaa bukta wanajaribu kuhoji kwanini yeye hajapigwa faini wakati ni tukio la siku moja (mechi baina ya Yanga na Ruvu Shooting). Ufafanuzi wangu kwenye hiyo picha ni kwamba yule sio kocha wa Ruvu Shooting bali ni kiongozi moja wapo wa Benchi la Ufundi ambapo katika hiyo mechi wasaidizi wa Salumu Mayanga walivaa sare rasmi za benchi la ufundi ambazo ndio hiyo inayoonekana kwenye picha huku kocha wao mkuu Mayanga akivaa Suruali ya jinsi na shati nyeupe.

Kuna picha ya benchi la ufundi la Manchester United siku za nyuma kidogo wakiwa wamevaa bukta na t-shirt nyeupe (jersey) za timu, kwa kifupi ile ilikuwa ni sare maalumu ya benchi la ufundi.

Kuna picha ya benchi la ufundi la Taifa Stars hii ya sasa ambapo viongozi wanaonekana wakiwa wamevaa bukta maalamu za benchi la ufundi lakini watu wanahoji hao vipi mbona hawajaadhibiwa? Jibu ni kwamba; (1) ile ni sare maalumu ya benchi la ufundi ya Taifa Stars, (2) Kanuni za Ligi Kuu, Ligi Daraja la kwanza na Ligi Daraja pili hazitumiki kwenye mashindano ambayo Taifa Stars inashiriki kwani Bodi ya ligi hawana nguvu kisheria na kikanuni kusimamia Taifa Stars.

Hiki kifungu cha mavazi katika kanuni ya utaratibu wa mchezo ni mpya kama nilivyosema mwanzo ndio maana hatujasikia kocha kama Ndayiragije akiadhibiwa kwa kuvaa zile kaptura zake za msimu uliyopita.

Bila kuweka ushabiki wa aina yoyote ile kwa kutumia mazingira na tamaduni za kitanzania mtu mzima kuvaa ile kaptura ya Mwinyi Zahera na kutoka nje utaonekana muhuni au mtu usiyekuwa na hekima wala heshima katika jamii. Mara nyingi hizi kaptura za Zahera tunazivaa maeneo ya starehe kama bar.

Watu wanajaribu kufananisha Ligi nyingine na hii ya kwetu kwamba mbona hizo nyingine hazina kanuni au sheria zinazohusu mavazi kama hii kanuni yetu ndio inawezekana kwani nimeona mpaka picha za kina Gurdiola na cardet zao au kina Klopp na truck suit na kofia zao za Liverpool lakini hawajawahi kutozwa faini ya mavazi. Lakini hatujiulizi kwanini EPL kuna VAR na kwingine hakuna VAR?

Binafsi sioni tatizo kuweka kanuni hii inayohusu mavazi kwa Benchi la Ufundi lakini tatizo ninaloliona ni juu ya mapungufu yaliyopo kwenye kanuni husika kwa kushindwa kufafanua kwa kina aina ya mavazi ambayo ni nadhifu na yenye heshima maana kwa tafsiri ya KAMUSI YA KISWAHILI (TATAKI) inaeleza kwamba “nadhifu ni kupendeza” na swala la mtu kupendeza sio lazima aambiwe na jirani yake bali yeye akivaa nguo flani akajitazama kwenye kioo akiona amependeza aina shida. Hivyo kwenye vazi la heshima inategemeana na utamaduni wa eneo, taasisi au jamii flani. Mfano kwa wamasai kuvaa yale mashuka yao na kufunga “rubega” ni heshima na wanaonekana nadhifu katika jamii yao.

Mimi nyumbani kwa wazazi wangu mwanaume kutoka nje akiwa amefunga taulo ni utovu wa nidhamu lakini pia mwanamke akivaa suruali haruhsiwi kuingia kwenye malango ya wazazi wangu.

Niwakumbushe kidogo mwaka 2002 FIFA waliwapiga marufuku Cameroon kutumia jezi zao ambazo t-shirt zilikuwa zinaishia kwenye mabega wakati huo huo walikuwa wamezitumia kwenye michuano ya Mataifa huru ya Afrika. Sijui tunakumbuka au ndio wengi wanaowashambulia TFF walikuwa watoto.

Jambo la msingi Bodi ya Ligi pamoja na TFF waangalie namna ya kuboresha hiyo kanuni kwa kuweka vifungo vidogo vidogo vinavyofafanua kwa kina aina gani ya mavazi yasio nadhifu na yenye heshima kutumiwa na benchi la ufundi.

Naamini hii adhabu ya Zahera angekuwa amepigwa kocha wa Namungo, Kagera Sugar, Geita Gold, Biashara United, Pamba, Toto Afrika au timu yoyote nje ya Simba na Yanga tusingesikia hizi kelele ila kwa vile rungu limetua kwa Yanga basi TFF wataambiwa ni hujuma kwa Yanga lakini pia kama ingekuwa adhabu ya kocha wa Simba basi ingeonekana ni hujuma kwa Simba.

Nimalize kwa kusema kwamba hii kanuni hajatungiwa Zahera kama ambavyo wengi wanasema kwani hata Ndayiragij

e alikuwa anavaa pensi ambazo sio rasmi tangu akiwa Mbao 2017/2018 ila kwa vile anafundisha vilabu ambavyo havina mashabiki wengi na wapiga kelele basi haongelewi sana.

Mwisho wa siku Yanga wanahusika kwenye adhabu ya Zahera na ndio maana viongozi wako kimya juu ya hili.

Asanteni,

+255716605949

Leave a Comment