breaking news New
Simba Mna Deni la Watanzania ni Kweli Ratiba ya TPL Kigugumizi

Simba Mna Deni la Watanzania ni Kweli Ratiba ya TPL Kigugumizi

USHINDANI wa Ligi Kuu Bara umeibuka ghafla hiyo ni baada ya timu kongwe za Simba na Yanga kuanza kukimbizana na muda kuhakikisha zinafanya vizuri msimu huu na kuwa bingwa ili msimu ujao mmoja wao aiwakilishe Tanzania kwenye michuano ya kimataifa.

Hapo kati kulikuwa na mechi za ligi hiyo, lakini kwa kiasi kikubwa kama ilipoteza mvuto kutokana na Simba kutocheza, huku Yanga ikiendelea na mechi zake za ligi hiyo.

Mashabiki wa Yanga wakawa wanatamba huku wale wa Simba wakiwa wapole kutokana na kuachwa pointi nyingi na kuwa na viporo vingi ambavyo hawakuwa na uhakika kwamba wanaweza kushinda vyote.

Baada ya juzi Alhamisi kushinda dhidi ya Mwadui, Simba wameamka na kuamini kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa wao kushinda mechi zao zote za viporo na kuwakamata Yanga na kuwapita kabisa Yanga hapo juu walipo.

Katika msimamo wa ligi hiyo kwa sasa, Yanga inaongoza ikiwa na pointi 55, Azam ni ya pili na pointi 48, huku Simba ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36. Tofauti ya mechi kati ya Simba na Yanga ni saba. Simba imecheza mechi 15 na Yanga 22.

Kwa sasa tunaweza kusema kwamba ligi imenoga kwa sababu ukiangalia ratiba ya mechi zijazo, zipo mfululizo kutokana na timu nyingi hazijacheza na msimu unatakiwa kumalizika Mei, mwaka huu.

Ni miezi takribani mitatu imebaki ili msimu umalizike, hivyo inafanyika juhudi kuona kasi ya sasa inaendana na muda uliobaki.

Timu zimeshaanza kulalamika juu ya ratiba ilivyobana. Zinasema kwamba ni ngumu na itawanyima fursa ya kufanya vizuri na mipango yao ya kumaliza ligi nafasi nzuri itavurugika.

Tunahitaji kuona ushindani huu uliopo sasa uwe endelevu mpaka mwisho wa ligi ili bingwa akipatikana kila mmoja ajue kweli amefanya kazi ya ziada. Siyo kubebana mwisho wa siku kwenye michuano ya kimataifa timu inaishia hatua za awali.

Ukiangalia kwa msimu uliopita ambao Simba ilikuwa bingwa wa ligi hiyo, timu hiyo ilikuwa imejipanga kisawasawa, utaona mpaka inajihakikishia ubingwa, ilikuwa haijapoteza hata mechi moja.

Kwa msimu mzima wa ligi hiyo ambao timu hiyo ilicheza jumla ya mechi 30, ilipoteza mechi moja pekee na mechi hiyo ilikuja baada ya kujihakikishia ubingwa.

Hivi sasa ukiangalia kinara Yanga ambaye amecheza mechi 22, tayari amepoteza mechi moja. Kuna kitu cha ziada Yanga inatakiwa kufanya ili kuilinda nafasi yake hadi mwisho wa msimu. Wakizubaa watashangaa wanashindwa kufikia malengo yao.

Nikiachana na ligi, upande wa michuano ya kimataifa, Jumanne ijayo, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba, watacheza dhidi ya Al Ahly kutoka Misri.

Mchezo huo wa nne katika hatua ya makundi ya michuano hiyo, utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kumbuka Simba imepangwa Kundi D na timu za AS Vita Club ya DR Congo, JS Saoura ya Algeria na Al Ahly kutoka Misri.

Msimamo wa kundi hilo, Al Ahly inaongoza ikiwa na pointi saba, AS Vita Club inafuatia na pointi nne, Simba inazo tatu na JS Saoura ya mwisho na pointi mbili. Bado mechi tatu kwa kila timu.

Bado tunakumbuka ahadi mliyoiweka kwamba mtashinda mechi zote za nyumbani. Baada ya kuifunga JS Saoura hapa nyumbani, sasa mwendelezo huo uwepo katika mechi dhidi ya Al Ahly na AS Vita Club ambapo mechi hizo zote zitachezwa hapa nyumbani.

Kumbukeni hilo ni deni ambalo mlituahidi, awali mlituahidi kwamba msimu huu mnataka kufika hatua ya makundi, kweli mmefika, sasa ni muda wa kulipa hili deni lingine.

Niwatakie maandalizi na mchezo mwema kwani mafanikio yenu ni mafanikio ya Tanzania kwa jumla. Watanzania tupo nyuma yenu katika kuhakikisha mnafikia malengo mliyojiwekea.

Kutoka Championi

Leave a Comment