Kwa heri Peter Cech GLOVES zako zitaendelea kukumbukwa Darajani

Kwa heri Peter Cech GLOVES zako zitaendelea kukumbukwa Darajani

Wakati zilipovuja taarifa za golikipa wa Jamhuri ya Czech ambaye alikuwa asajiliwe na klabu ya Manchester United atakwenda Chelsea kwa sababu mtu ambaye alikuwa amesimamia deal ya usajili wake Old Trafford Peter Kenyon alikuwa anakwenda kwenye mapinduzi ya Kirusi huko Stamford Bridge si watu wengi walikiona walichokipoteza United.

Petr Cech ambaye United ilikuwa umetazama kama mrithi sahihi wa Peter mwingine, alijiunga Chelsea na kilichofuatia baada ya hapo hadi January 15, 2019 ni historia kama wasemavyo wahenga.

Haikumchukua muda kuidhihirishia dunia kuwa alikuwa kipa bora wakati huo kwani katika msimu wake wa kwanza Cech alicheza dakika 1025 bila kuruhusu wavu wake kuguswa rekodi ambayo baadaye ilikuja kuvunjwa na Edwin van der Sar wa Manchester United na mpaka ulipofika mwisho wa msimu kipa huyo raia wa Jamhuri ya Czech aliweka rekodi nyingine ya kufungwa idadi ndogo ya mabao ambayo yakikuwa mabao 15 pekee.

Akiwa kwenye msimu wake wa pili ambapo alifungwa mabao 22 pekee kwenye mechi 34 za EPL Petr Cech alichaguliwa kuwa kipa bora duniani na taasisi inayotunza kumbukumbu na historia ya michezo mbalimbali ikiwemo soka la IFFHS.

Maisha ya Petr Cech kwenye soka la kulipwa la kiwango cha juu yalianzia kwao Jamhuri ya Czech kwenye klabu mbalimbali ikiwemo Sparta Prague ambayo aliichezea kwa msimu mmoja na kuhamia Ufaransa kwenye klabu ya Rennes ambako alidumu kwa miaka miwili kabla ya kuhamia Chelsea kwa ada ya uhamisho ya £7M ambayo kwa wakati huo ilimfanya kuwa kipa ghali kuliko wote kwenye historia ya Chelsea.

Wengi walihisi Cech asingeweza kurejea kwenye ubora wake katika msimu wa 2006 wakati alipopata ajali ya kugongana na beki wa Reading Stephan Hunt ajali ambayo ilimweka Cech nje ya uwanja kwa muda wa miezi mitatu na aliporejea alilazimika kuvaa kifaa maalum cha kumpa ulinzi wa fuvu lake ambalo lilihitaji upasuaji kurekebishwa baada ya kuvunjika kwenye sehemu ndogo kufuatia kishindo cha goti la beki wa Reading.

Hata hivyo Cech alipambana na kurudi uwanjani na kuendeleza ubora wake akiitumikia Chelsea kwa miaka mingine 9 baada ya hapo mpaka mwaka 2015 alipohamia Arsenal akipisha ujio wa kipa kinda Courtois ambaye Chelsea ilimrejesha kikosini kutokea Atletico Madrid.

Akiwa Arsenal kwenye msimu wake wa kwanza Cech alifanikiwa kuweka rekodi nyingine ya ligi akicheza mchezo wake wa 170 bila kuruhusu bao na kuivunjilia mbali rekodi ya awali iliyowekwa na David James miaka hiyo na msimu uliofuata alifanikiwa kutwaa ubingwa wa kombe la FA ambao kwake binafsi ulikuwa wa 5 baada ya kutwaa na Chelsea mara nne kabla.

Hadi anatangaza kustaafu Cech alitwaa ubingwa wa EPL mara 4 kombe la FA mara 5 na mataji ya Ulaya ambayo ni ligi ya mabingwa na UEFA Europa League.

Kauli ya nahodha wake wa zamani John Terry ya kwamba Cech kwa mikono yake alizisaidia timu alizocheza walau kuvuna pointi 15 zaidi inadhihirisha ubora ubora wake na ndio maana mkongwe wa England Peter Shilton hakusita kuikumbisha saa chache baada ya gwiji huyo kutangaza kuachana na soka mwishoni mwa msimu huu na bila shaka ataendelea kukumbukwa hata kwenye klabu ya Chelsea ambayo imetangaza nafasi ya ukocha na ubalozi kwa kipa huyo baada ya kutundika gloves zake.

Leave a Comment