Asante Kipa tegemeo David De Gea kwa utamu huu!!

Asante Kipa tegemeo David De Gea kwa utamu huu!!

Katika ukurasa wake wa tweeter mwanaume mmoja mabaye wengi walidhani ndiye aliyewahi kuvaa gloves bora kwenye kikosi na historia ya Manchester United alikuwa ameweka emoji ya kunyoosha mikono juu akikubali kazi ya David De Gea, anaitwa Peter Schmeichel alikuwa anashuhudia De Gea akizuia michomo 11 dhdi ya Spurs na kuwapa Manchester ushindi wa 6 mfululizo tangu wawe chini ya Super Sub Ole Gunnar Solskjaer.

Inawezekana dunia ikawa haikuguswa kwa kiwango kikubwa na kiwango chake kama ilivyo kama ilivyokuwa kwa kocha wa Manchester United Ole, akiwa na sura yenye hisia sura iliyoonekana kuzungumza kutoka moyoni na midomo ikiwa na uzito wa kutoamini kama alikuwa anayasema yale.

Solskjaer alikuwa anaweka hadharani kuwa, inawezekana muda sio mrefu De Gea akapewa ufalme kati ya magolikipa waliowahi kuvaa jezi ya United.

Huyu anaweza kuwa kipimo kizuri kwani ni wazi aliwahi kucheza kwa nyakati tofauti na wanaume wa shoka waliowahi kusimama katika milingoti ya Si Alex Ferguson yaani Edwin van der Sar na Peter Schmeichel.

Pengine katika akili ya kawaida tukawa tunawaza ukubwa wa Lionel Messi na umuhimu wake kwenye kikosi cha Barcelona au labda tukakimbilia Seria A na kuitazama namna ambavyo Ronaldo anavyobadilisha falsafa nzima ya Juve lakini kuna ukweli mmoja tu, ni ngumu duniani kote golikipa kuwa mchezaji bora wa klabu.
Katika kuongeza sukari katika keki hii ya De Gea amekuwa mchezaji bora wa Manchester United mara 4 katika miaka 5 iliyopita. Wakati hayo yakitokea kikosi cha Manchester United kilikuwa na Rooney, alikuwepo Zlatan, akafika Pogba na hata miguu ya wachezaji walioaminika kuja kufanyamakubwa kama Martial na Rashford haikuwahi kuzungumzwa kwa kiwango chake.

Inawezekana kwenge mboni za wapenzi wengi wa soka kukawa na magolikipa wengi wazuri kwa kipindi hiki, unaweza kuwawaza Jan Oblak, Alisson Becker pia ukapata fikra kumfikiria Thibaut Courtois na wapo wanaoamini katika Marc-Andre ter Stegen
lakini kuna tofauti moja ambayo De Gea anayo kulinganisha na wote.

Amekuwa mchezaji bora zaidi kwa Manchester United katika misimu 6 iliyopita inawezekana pia wakawepo wale wanaosema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita Sir Alex Ferguson hakuwahi kufunga ndoa bora kama hii aliyoileta na De Gea, iitwe takaifu kwenye soka.

Uso wa dunia umegubikwa na ufalme wa magoli ya Ronaldo, Messi, Salah na wengine wengi lakini De Gea ni mwanaume mmoja anaepigania nafasi ya ufalme kwa nguvu na baraka iliyoko kwenye mikono yake.
Yawezekana pia haya yote yanatokana na ukweli kuwa Manchester United kwa miaka ya hivi karibuni haijawahi kuwa na ujasiri mzuri wa kupata wachezaji watakaokuwa kwenye uso wa dunia.

Lakini ni wangapi wanaweza kuishi kwenye kiwango cha De Gea kwa misimu yote tangu alipoletwa akiwa mtoto 2011? Wakati Alisson akifichiwa ubora wake na Virgil van Dijk na Salah. Ter Stegen akisahaulika kutokana na ufalme wa Messi, Oblak akiwa anasubiri Griezmann azungumzwe kwanza, pale Carrington mfalme ni David De Gea.

Pogba anafungua mlango ili apite Nemanja Matic anapisha kitini ili aweze kuketi na Martial anainama ili kumsalimia ameketi kwenye kiti cha enzi na wakati huu ambao ambao tunawaza nani mkali kati yake ukilinganisha na magwiji Edwin van der Sar na Peter Schmeichel jina lake linaendelea kuandikwa kwa mhuri wa moto.

Miaka 10 baadaye tutapata nafasi ya kusimulia kuwa alikuwepo mwanaume ambaye angeweza kufanya takwimu za mabeki zako zipande, mwanaume ambaye alikuwepo mfalme pasipo kufunga magoli, mwanaume ambaye hakusifika kwa style yake ya mavazi na nywele lakini kwa gloves alizokuwa anavaa.

Peter Schmeichel alicheza Manchester United kwa misimu 9, mechi zinazofika 300, Van de Sar alicheza kwa misimu isiyozidi 6 na hakufikisha mechi 200. De Gea tayari amecheza mechi 259 na ndio kwanza ana miaka 28 anayo misimu zaidi ya mitano ya kuendelea kuwa imara iwapo ataepuka majeraha anaomuda wa kusimika historia yake na anaomuda wa kuendelea kutufanya tufurahie maajabu ugolikipa.

Wakati mwingine sio shuti la Messi au tiktak ya Ronaldo pekee kuna wakati balaa linafanywa na sare ya golikipa.

Asante David De Gea kwa utamu huu.

Leave a Comment