Alichofanya Manara kilipaswa kufanywa na Simba

Alichofanya Manara kilipaswa kufanywa na Simba

Haji aliingia Simba kama mtu wa kawaida sana alikua mtu anayejulikana na watu wachache ila hakuwa maarufu, amewahi kupita Radio Uhuru lakini si wengi walimjua huko amewahi pia kupita CCM lakini si wengi walimfahamu, na aliwahi pia kuambatana na Sheikh Mazinge kwenye mihadhara lakini hakupata umaarufu sana maana alifunikwa na Mazinge mwenyewe.

Ingawa mwenyewe hujinasibu kuwa alikua Star tangu alipokua mchanga, kwamba magazeti yaliandika kuhusu kuzaliwa kwake ila ukweli ni kuwa yeye Haji hakua Star bali baba yake Sunday Manara ndie aliyekuwa Star.

Wakati uongozi wa Simba chini ya Rais Evance Aveva wanamchukua Haji hawakuzingatia kama ana taaluma ya Uafisa Habari waliachoangalia ni uwezo wake mkubwa wa kuzungumza.

Sina hakika kama alipeka hata vyeti ila nachokumbuka Simba walimhitaji sana Haji kwani klabu ilikua imepooza afisa habari aliyekuwepo kipindi hicho alikua mpole sana huku watani wao wa jadi Yanga wakiwa na Jerry Muro.

Haji akaanza kazi akashindana na Muro akamshinda akajizolea umaarufu, akamvaa hadharani Rais wa TFF wa wakati huo Jamal Malinzi, umaarufu ukazidi kwa Haji na akaaaminika sana kwa wana Simba.

Wakati fulani Simba walikuwa na timu mbovu lakini Haji akawaamisha Simba kuwa wamekosa ubingwa kwa sababu ya kuonewa, wanasimba wakaamini na akawachota akili eti waandamane kwenda Waziri.

Alichotumia Haji ni vitu viwili tu taaluma yake ya Propaganda na sauti yake nzito yenye mamlaka.

Ghafla Haji akawa mkubwa kuliko klabu,  Simba ikifungwa analaumiwa yeye.

Kuna watu hawamjui Rais wa Simba Sweddy Nkwabi wanamjua Haji.

Ukubwa wa Haji dhidi Simba umethibitika mitandaoni wapo watu hawajui ukurasa rasmi wa Instagram wa Simba lakini wanaujua wa Haji.

Namba hazidanganyi Instagram ya Haji ina wafuasi 798K lakini Instagram ya Simba  inawafuasi 458K, sitaki kuingilia kama Haji anaitumia Simba kwa manufaaa yake au la, lakini ukweli ni kuwa jamaa kanufaika sana na Simba na hatimaye sasa amekua star halisi.

Baada ya Haji kujigundua kuwa ni ‘Brand’ ameanza kutumia vema u-star wake, ameanza kufanyia biashara Brand yake.

Haters wanasema eti biashara sio zake hiyo haijalishi kwanini wasikupe wewe, kwa wale waliosoma Commerce kidato cha pili watakumbuka somo la hisa (SHARE) kwamba ukitoa jina lako litumike kwenye biashara nawe pia ni mwanahisa.

Turudi kwenye mada, alichofanya Haji kilipaswa kufanywa na Simba wenyewe, Simba ilitakiwa iwe na biashara zake, ukisoma katiba ya  Sunderland (Simba) ukurasa wa kwanza kwenye malengo ya klabu (OBJECTIVE) inasema klabu itanunua ardhi na kujenga majengo ya kibiashara, kisha kupangisha au kuuza, yaani wanachofanya NSSF leo, Simba walipanga kukifanya tangu  miaka ya 1930.

Simba imelala na Haji hakutaka kuwaamsha maana angewaamsha angelala yeye au wangelala wote.

Wapo wakosoaji wanaosema sio mawazo yake kuna watu nyuma yake lakini ukweli ni kuwa hao watu wamemfuata baada ya yeye kuwa Star.

Go Haji tumia vizuri jina lako usigeuke nyuma wakisema unajinufaisha usiwajali sana hujaanza wewe kunufaika na Simba, nasikiaga kuna watu wanauza jezi za klabu na klabu haipati chochote sembuse wewe unatumia jina lako.

Cha msingi sasa umekua mfanyabiashara punguza kuwakebehi mashabiki wa soka, hao sasa sio tena wanachama wa Simba wala Yanga,  hao ni wateja wako ukiwazingua hawatanunua Perfume yako.

Punguza kuwakera, nani atakubali umuite Mbutembute au Gongowazi halafu anunue perfume yako?

Mwandishi: Ahmed Ally

Leave a Comment